emblem

TANZANIA INDUSTRIAL RESEARCH AND DEVELOPMENT ORGANIZATION

TIRDO for sustainable industrial development

News

MAFUNZO YA NAMNA BORA YA UZALISHAJI MKAA MBADALA

  • 2023-10-10 09:10:16

Article Image

Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa masuala ya Kiuchumi na Umaskini (REPOA) wameanza kuwajengea uwezo wajasiriamali wanaojihusisha na kutengeneza mkaa mbadala ili wafahamu uzalishaji bora wa nishati hiyo. Hatua hiyo ni utekelezaji wa mwongozo wa nchi wenye lengo la kuhakikisha kunakuwa na nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030. Akizungumza Septemba 12,2023 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uzalishaji mkaa mbadala kwa wajasiriamali, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Profesa Mkumbukwa Mtambo, amesema yameshirikisha wazalishaji 22 kwa lengo la kuwaongezea ujuzi na ufahamu wa uzalishaji bora wa mkaa safi. “Mafunzo haya yametayarishwa baada ya kufanyika utafiti katika mikoa 12 hapa nchini na kutembelea wazalishaji mkaa mbadala 58 na watumiaji 122. “Utafiti ulifanywa na TIRDO kwa kushirikiana na REPOA ukiwa na lengo la kuimarisha uzalishaji wa mkaa mbadala na kukuza matumizi yake kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi nchini. Amesema watafiti walichukua sampuli 43 za mkaa mbadala kutoka kwa wazalishaji katika mikoa hiyo na kupima kwenye maabara ambapo matokeo ndiyo yaliyopelekea mashirika hayo kufanya uboreshaji baada ya kubaini changamoto za viwango na ubora unaotakiwa. Mkurugenzi huyo amesema pia watafiti wameweza kusanifu mashine ya kuchomea malighafi za bayomasi yenye uwezo wa kupunguza niashati ya kuchomea kwa asilimia 50, kuvuna joto ambalo linatumika kukaushia mkaa na kuvuna vinega. Mkurugenzi Mkuu wa REPOA, Dk. Donald Mmari, amesema wamebaini wazalishaji wengi hawana ujuzi wa kutosha kuzalisha mkaa mbadala wenye viwango vinavyokubalika. Amesema mkaa mbadala utasaidia kutunza mazingira na misitu kwa sababu asilimia 85 ya Watanzania wanatumia mkaa unaotokana na miti. “Unapokuwa na mkaa mbadala tutaokoa sehemu kubwa ya misitu yetu na kusaidia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa ambayo inachangia kwenye mabadiliko ya tabianchi na kuleta athari kubwa,” amesema Dk. Mmari. Mwenyekiti wa Wazalishaji na Wasambazaji wa Nishati Safi Tanzania, Phinias Magesa, amesema bado kuna changamoto ya kutambuliwa kwa teknolojia ya uzalishaji nishati mbadala. “Watu wanaozalisha teknolojia kama hizi wanaonekana hawana chochote lakini wana mchango mkubwa sana, tunashukuru Serikali imekuwa sikivu na wameanza kuwatambua wazalishaji wa mkaa mbadala…tukijikita katika mkaa mbadala tutapunguza ukataji miti,” amesema Magesa.